Friday, May 24, 2013

Maadhimisho ya Miaka 50 ya OAU Dar es salaam, Tanzania

Mheshimiwa Waziri Bernard Kamillius Membe akiwasha mwenge wa maadhimisho ya miaka 50
ya Umoja wa Afrika

Dar es salaam, Tanzania 



Mhe. Bernard K. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, leo ameongoza Watanzania na Jumuiya ya Mabalozi wa Afrika walioko nchini kuadhimisha
miaka 50 ya OAU/ AU. 

Maadhimisho hayo yameanza kwa kuwasha mwenge na kufuatiwa na maandamano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa yaliyohitimishwa kwenye Ukumbi wa Karimjee.

Sambamba na maandamano hayo, kumefanyika mhadhara wa wazi kwenye ukumbi wa Karimjee uliojadili Umajumui(pan-africanism), mwamko mpya wa Afrika ( African Renainsence) na ushiriki wa Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika. 

Katika hotuba yake, Waziri Membe amesifu mafanikio ya OAU kuwa ni kuwaunganisha waafrika na ukombozi wa bara la Afrika kutoka kwa wakoloni. Afrika imebaki na deni
moja la Sahara Magharibi ambapo Tanzania inaendelea kuhimiza juu ya haki yao ya kujitawala na kufuatilia kwa karibu mazungumzo yanayoendelea.

Aidha amezungumzia mafanikio katika kujenga demokrasia barani Afrika. Amesema leo karibu nchi zote za Afrika zinafanya chaguzi ikilinganishwa na miaka 30 iliyopita
ambapo kulitokea mapinduzi katika nchi 32. 

AU imevunja mwiko wa kuchelea kuingilia masuala ya ndani ya nchi pale demokrasia na haki za binadamu zinaposiginwa. AU imepitisha Azimio la Kutotambua Serikali zinazoingia kwa mapinduzi. Ni kwa sababu hizo, Tanzania na nchi marafiki ziko DRC kudhibiti vikundi vya waasi na kulinda
amani na haki za binadamu.

Mhe Waziri amepongeza jitihada za AU katika kutatua migogoro ya Afrika pamoja na changamoto inazokumbana nazo. Ameitaka dunia kuiunga mkono AU na kuisaidia bila
kuiingilia katika majukumu yake. 

Amemalizia kwa kuhimiza umuhimu wa Afrika kujikomboa kiuchumi kwa kujenga miundombinu na kukuza biashara miongoni mwa nchi za kiafrika. Amehimiza umuhimu wa
kuimarisha jumuiya za kikanda ili kujenga uchumi imara.

Maandamano yakipokelewa kwenye Viwanja vya Karimjee

Mheshimiwa Waziri na Mabalozi wakiimba wimbo wa AU na wimbo wa Taifa

Mheshimiwa Waziri Membe akiwasilisha hotuba yake ya ufunguzi.

Sehemu ya Wahudhuriaji wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya AU ndani ya ukumbi wa Karimjee