Friday, January 18, 2013

Mkuu wa Itifaki wa Marekani amuaga Balozi Maajar


Balozi Capricia Penavic Marshall, Mkuu wa Itifaki wa Marekani akitoa maelezo kuhusu utendaji kazi wa Balozi Maajar wakati wa hafla fupi aliyoiandaa ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa heshima ya Balozi Mwanaidi na Bw. Shariff Maajar. 

Balozi Marshall akisoma waraka kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Rodham Clinton, akimtakia kila la kheri Balozi Maajar, ambaye anamaliza muda wake wa uwakilishi nchini Marekani.

Mkuu wa Itifaki wa Marekani Balozi Marshall leo amesema Balozi Mwanaidi Maajar amefanya kazi kubwa ya kudumisha mahusiano baina ya Marekani na Tanzania na Jumuiya ya Wanadiplomasia hapa Washington DC watamkumbuka kwa hilo.


Aliyasema hayo kwenye hafla fupi ya chai ya asubuhi aliyoiandaa kwa heshima ya Balozi Mwanaidi Maajar na Bw. Shariff Maajar wanaotarajia kurejea nchini Tanzania baada ya kumaliza muda wa uwakilishi nchini Marekani. 

Miongoni mwa mambo ambayo Balozi Marshall ameyataja kuhusu Balozi Maajar ni kile alichokiita uwezo wake mkubwa wa kazi ya uwakilishi akitoa mfano wa Balozi Maajar kuuliza maswali yanayohusu mahusiano baina ya Marekani na Tanzania kwenye ziara zote zilizoandaliwa na mkuu huyo wa itifaki kwenye majimbo mbalimbali ya Marekani. 

"Kila mara tunapokuwa safarini, sehemu ya maswali ikifika, Balozi Maajar yeye huwa wa kwanza kwenye kipaza sauti na kuuliza maswali au kuchangia mazungumzo ili kuhakikisha mahusiano ya nchi zetu mbili yanakua" alisema Balozi Marshall.

Alichukua pia nafasi ya kusoma waraka ulioandikwa na Mhe. HIllary Rodham Clinton, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akimtakia Balozi Maajar kila la kheri na mafanikio mengi mara arudipo Tanzania. 

Balozi Marshall alisisita amefurahi sana kupata fursa ya kufanya kazi na Balozi Maajar na japokuwa anarudi Tanzania, lakini msingi wa mahusiano baina ya nchi hizi mbili utaendelea kudumu daima, na yeye binafsi anajua anarafiki Tanzania. 

Kwa upande wake Mhe. Maajar alielezea mafanikio yaliyopatikana katika kuendeleza mahusiano baina ya nchi mbili. Pia aliishukuru serikali ya Marekani kwa programu mbalimbali zinazoendelea Tanzania zikiwemo mpango wa kutokomeza malaria, UKIMWI, lishe bora kwa mama na mtoto na kilimo. 

Alitangaza kuwa Mkataba wa pili wa Milenia au Millenium Challenge Compact umepitishwa huu ukiwa ushahidi tosha wa ushirikiano baina ya Marekani na Tanzania ambapo Watanzania wengi watanufaika nao hususan kwenye upande wa kuboresha miundo mbinu, kilimo, elimu na afya.

Akinukuu maneno ya Rais Kikwete ambaye amemuwakilisha nchini Marekani kwa miaka miwili, Balozi Maajar amesema, "Tunathamini sana uhusiano wetu na watu wa Marekani, hivyo nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuhakikisha mahusiano yetu yanakua". 

Balozi Maajar alimuomba Balozi Marshall afikishe salamu zake za shukrani kwa Mhe. Hillary Clinton kwa jitihada zake kubwa za kuitangaza sera ya Mambo ya Nje ya Marekani huku akitoka kipaumbele kwenye masuala ya maendeleo ya wanawake. 

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali hususan za kiafrika na baadhi ya wafanyakazi  wa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na marafiki, ilifanyika kwenye chumba cha James Monroe, ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliyopo mtaa wa C, mjini Washington D.C.

Balozi Mwanaidi Maajar akikabidhi zawadi ya Mama Hillary Clinton kwa Mkuu wa Itifiaki Balozi Marshall na kuelezea zawadi hiyo ambayo ni khanga yenye maandishi "Hongera Barack Obama" na picha ukutani aina ya tingatinga

Balozi Maajar akishukuru kwenye hafla maalum ya kumuaga iliyohudhuriwa na baadhi ya Mabalozi wa nchi mbalimbali zikiwemo za kiafrika.


Balozi Maajar akisindikizwa na mumewe Bw. Shariff Maajar akimkabidhi Balozi Marshall zawadi ya khanga kutoka Tanzania wakati akitoa shukrani zake kwenye sherehe ya kumuaga. 





Balozi Maajar akiagana na Afisa Dawati la Tanzania wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ellen Peterson wakati wa sherehe ya kuaga iliyoandaliwa kwa heshima yake.