Milwaukee, WI: Meya wa Milwaukee
kwenye Jimbo la Wisconsin amemtunukia Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe.
Mwanaidi Sinare Maajar hati ya kuitambua siku ya tarehe 20.02.2012 kama siku ya
Tanzania mjini Milwaukee.
Mayor Thomas Barrett ametangaza
siku hiyo ofisini kwake leo (jana) kama sehemu ya kuipongeza Tanzania kwa
kutimiza miaka 50 ya uhuru na kuendeleza ushirikiano baina ya miji dada (sister
cities) ya Milwaukee nchini Marekani na Morogoro nchini Tanzania.
Katika hafla hiyo
fupi iliyohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, Meya Barrett
na Balozi Maaajar walikubaliana kuendeleaza ushirikiano baina ya miji hii
miwili, ulioanzishwa mwaka 2006, na pia kushawishi wawekezaji na wafanya
biashara wa ukanda huu wa Marekani kuwekeza Tanzania.
Balozi Maajar yuko
Jimboni Wisconsin kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu iliyoandaliwa na muasisi
wa ushirikiano wa miji ya Milwaukee na Morogoro Bw. Ryan Skyfe, ambapo
anakutana na taasisi za elimu, biashara na wawekezaji mbalimbali kwa nia ya kuangalia
maeneo ya ushirikiano wenye tija ili kuleta maendeleo kwa manufaa ya wananchi
wa nchi hizo mbili.
Baadhi ya taasisi
alizofanya nao mazungumzo ni Milwaukee Area Technical College walioko kwenye Jimbo
la Wisconsin mjini Milwaukee ambao wamekubali kushirikiana na mojawapo ya chuo
cha Tanzania na kutoa elimu inayolingana na mitaala ya chuo hicho ambacho
kinaongoza kwenye Jimbo hili kwa kutoa elimu ya vitendo kwenye sekta ya nishati
ya umeme inayowasaidia Wamerekani kupata ajira.
Wengine ni Phoenix
Financial & Investment Services walioko Jimbo la Illinois mjini Chicago na
Helios Solar Works walioko Jimbo la Wisconsin Mjini Milwaukee. Balozi Maajar
pia alipata fursa ya kutoa mada kwenye mkutano uliovutia wakuu wa biashara na
wawakilishi wa makampuni wapatao thelathini kutoka kwenye Jimbo la Wisconsin
wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania.
Aidha Balozi Maajar
alitumia fursa hiyo kuirajamu Tanzania na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo
baina ya serikali za nchi hizi mbili kwa wananchi wake kuwekeza na kuendeleza
ushirikiano kwa manufaa yao.
Kila mwaka Balozi wa
Tanzania nchini Marekani huandaa ziara
mahsusi kwa ajili ya maafisa wakuu wa makampuni ya kimarekani kutalii Tanzania na kuangalia fursa
za uwekezaji na biashara nchini Tanzania. Ziara hiyo ambayo inachanganya
biashara na utalii (business and leisure) imekuwa mashuhuri sana miongoni mwa
wafanyabiashara wa Kimarekani ambapo mwaka huu inatarajiwa kufanyika tarehe 22
Juni – 02 Julai, 2012.
Balozi Maajar kesho tarehe
21.02.2012 anatarajia kukutana na Gavana wa Jimbo la Wisconsin Mjini Madison na
baadae kuendelea na ziara yake kwenye miji ya La Farge na La Crosse Jimboni
Wisconsin kabla ya kurejea mjini Washington, jimbo la District of Columbia.
Mindi
Kasiga,
Wisconsin, Marekani.
20.02.2012